User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imezindua majengo mawili jijini Paris, Ufaransa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mahsusi wa kumiliki majengo ya Serikali nje ya nchi.

Majengo hayo ya ofisi ya Ubalozi na makazi ya Balozi yaliyogharimu Serikali Euro milioni 22, yalizinduliwa rasmi na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Wanadiplomasia na Watanzania jijini Paris tarehe 28 Januari 2015.

Uzinduzi wa majengo hayo yenye ukubwa wa ghorofa nne kila moja na sehemu ya chini ya ardhi ya maegesho ya magari ni mafanikio ya Sera ya Mambo ya Nje ambapo kupitia mkakati wake wa miaka 15 wa kumiliki majengo nje ya nchi, umefanikisha mchakato wa manunuzi ulioanza mwaka 2012.

“Niwapongeze Wizara ya Mambo ya Nje kwa kufanikisha zoezi la ununuzi wa majengo haya kutoka Serikali ya New Zealand ambao ni marafiki zetu wa kweli wa maendeleo na niwashukuru kwa kutuvumilia wakati wote huu” alisema Rais Kikwete.

rais jakaya kikwete mama salma kikwete waziri membe balozi taj
Mhe. Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete kwneye picha ya pamoja na Waziri Bernard Membe na Balozi Begum Taj mara baada ya kuzindua majengo ya Serikali jijini Paris Ufaransa tarehe 28 Januari 2015.

Akimkaribisha Rais kutoa hotuba yake, Mhe. Bernard Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje alisema umiliki wa majengo hayo ya Serikali jijini Paris ni uthibitisho wa ukomavu wa diplomasia ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Mheshimiwa Rais, ulituagiza kununua majengo jijini Washington D.C., tulifanya hivyo, jijini New York, tulifanya hivyo na sasa jijini Paris, tumetekeleza. Mkakati wetu ni kukamilisha maeneo ya kipaumbele ambapo sasa tuko mbioni kukamilisha mchakato wa kujenga kitega uchumi jijini Nairobi na Maputo” alisisitiza Waziri Membe.

Mkakati wa miaka 15 wa kumiliki majengo ya Serikali nje ya nchi unapata nguvu kutoka kwenye Sera ya Mambo ya Nje yenye muelekeo wa uchumi uliobuniwa mwaka 2002/03 japo utekelezaji wake ulianza rasmi mwaka 2007/08 baada ya Serikali kuanza kutenga fedha za miradi ya maendeleo kwa Wizara ya Mambo ya Nje.

Licha ya ununuzi wa majengo, mkakati huu pia unahusisha ujenzi na ukarabati wa majengo ya ofisi, nyumba za watumishi wa Serikali na kuendeleza viwanja vinavyomilikiwa na Serikali kwenye maeneo ya uwakilishi.

“Ununuzi wa majengo haya ni mafanikio makubwa. Sio tu imepunguzia Serikali mzigo wa kodi, lakini imetuwekea heshima kubwa hapa Ufaransa sisi kama nchi. Kama mjuavyo Ufaransa pia ni mojawapo ya Super Power (mataifa yenye nguvu), ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hivyo Tanzania kumiliki majengo ya kudumu jijini Paris ni ishara ya ukomavu wa diplomasia yetu” alihimiza Mhe. Taj Begum, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.

Hivi sasa Serikali kupitia Balozi zake nje ya nchi inamiliki majengo 97 ndani ya vituo 32 zikiwemo ofisi za ubalozi na nyumba za watumishi. Ifikapo mwaka 2017 wakati wa ukomo wa mkakati huu, namba hii itapanda zaidi hususan kwenye upande wa ofisi za Ubalozi.

Na Mindi Kasiga,
Paris, Ufaransa
29 Januari 2015